*Ugonjwa usipodhibitiwa
unaharibu macho, moyo, figo, misuli, ufanisi kiuchumi
Mwandishi Wetu, TJNCDF
KISUKARI ni ugonjwa unaoonyesha viwango vikubwa
vya glukosi katika damu. Sababu yake ni uhaba
wa homoni ya insulini mwilini au upungufu
wa uwezo wa mwili wa kukubali insulini.
Kuna watu wanaozaliwa wakiwa hawana insulin hiyo inayochochea
matumizi ya sukari, hivyo kuwa na kisukari cha utotoni na kuna wanaokipata
kutokana na mwenendo wa tabia za maisha.
Vile vile, kuna wanawake wanaokipata wakati wakiwa wana mimba
lakini baada ya kujifungua hupana na mwili wao unarejea katika hali ya kawaida.
Kwa ujumla ugonjwa wa kisukari hutokana na kiwango kikubwa
cha sukari kwenye damu kuliko inavyotakiwa au kuna mkwamo wa matumizi mwilini.
Sukari kwenye damu ikizidi viwango vya kawaida kwa muda mrefu husababisha
madhara mengi mwilini.
Chama cha Ugonjwa wa Kisukari (TDA) katika taarifa yake juu
ya “nini ufahamu kuhusu ugonjwa wa kisukari’ kinasema sukari mwilini hutokana
na vyakula pamoja na vinywaji ambavyo mtu anavitumia kila siku na kazi yake
kubwa ni kuupa mwili nguvu.
Athari za ugonjwa wa
kisukari
Ugonjwa wa kisukari unasababisha athari nyingi mwilini.
Miongoni ni pamoja na magonjwa ya moyo kuwa zaidi ya mara mbili zaidi ya watu
wasio na ugonjwa huo.
Matatizo mengine ni shinikizo la damu, kiharusi, kuharibika
mishipa ya damu na ile ya fahamu kiasi cha kusababisha ganzi, vidonda na hata
gangirini ya miguu. Takwimu zinaonyesha kwamba ugonjwa wa kisukari ni moja ya
sababu za watu wengi kukatwa miguu.
Ugonjwa wa kisukari pia husababisha kuharibika kwa figo na
kuzifanya kushindwa kufanya kazi. Pia husababisha matatizo ya macho na upofu.
Madhara mengine ni kupungua kwa kinga ya mwili na kuuweka
mwili katika hatari ya maambukizi ya ngozi, fizi, njia ya mkojo, uke na kifua
kikuu. Vile vile unaweza kusababisha kupungua nguvu za kiume, utendaji wa kazi
na kuathiri uchumi.
Dalili za Kisukari
Zipo dalili nyingi lakini miongoni ni kuhisi kiu mara kwa
mara, kwenda haja ndogo mara kwa mara, kuwa dhaifu, uchovu kila wakati,
kupungua uzito au kukonda.
Dalili nyingine ni kusikia njaa kila wakati, wanawake
huwashwa sehemu za siri, kutoona vizuri, kupungua nguvu za kiume, ganzi, kuhisi
kuchomwachomwa, miguu kuoza, vidonda na majeraha kutopona haraka na majipu
mwilini.
Namna ya kujikinga na
kisukari
Mwenyekiti wa TDA, Profesa Andrew Swai anasema mtu anaweza
kujikinga na ugonjwa wa kisukari kwa kupunguza unene kwani hupunguza uwezo wa
mwili kutumia sukari.
“Uzito wako usizidi urefu mara urefu mara 25. Kwa mfano mtu
mwenye urefu wa mita 1.63 uzito unatakiwa usizidi 1.63 x 1.63 x 25 ambayo ni
sawa na kilo 66. Urefu uwe kwa mita na uzito uwe kwa kilo.
Njia nyingine, anasema ni kujishughulisha mwili kwa kufanya
chocchote kitakachokufanya utoke jasho au moyo kwenda mbio kwa angalau nusu saa
kila siku, hata kama sii mnene.
Kujishughulisha ni kufanya jambo lolote la kutumia misuli
mwilini, kwa mfano kutembea, kukuimbia, kufanya kazi za nyumbani, kulima,
michezo mbalimbali na kucheza dansi.
Kujishughulisha ni muhimu sana kwa matumizi ya sukari mwilini
na afya kwa ujumla. Kukaa kwa muda mrefu bila kujishughulisha nako sii vizuri,
inatakiwa usikae zaidi ya saa moja bila kujishughulisha, kwa angalau dakika
mbili au tatu.
Njia nyingine ni kupunguza matumizi ya pombe au kuacha
kabisa, kutotumia sigara au aina yoyote ya tumbaku na kuepuka misongo ya
mawazo. Msongo wa mawazo ni kisababishi kikubwa cha kisukari na sukari kuzidi
kuwa juu kwa walio na kisukari.
Tunaweza kuepuka misongo mingi kwa kuwa wakweli kuhusu
mahitaji yetu ya lazima, uwezo wetu na muda tulionao. Tuna haja ya kuamua ni
kipi tuwaachie wengine au kushirikiana kwani mtu mmoja hawezi yote.
Njia ya mwisho lakini iliyo na umuhimu mkubwa ni kula chakula
inavyotakiwa. Sehemu kadhaa za mwili hufanya kazi muda wote tangu kuzaliwa hadi
kufa bila kupumzika. Viungo hivyo ni kama ubongo, mapafu, moyo na figo.
Hivyo mwili unahitaji sukari kila dakika. Kuwezesha hili,
vyakula vyote vimeumbwa vigumu; sio vya kumiminika, ili vitulie tumboni.
Tumbo linavisaga na
kuviachia kidogo kidogo kadiri mwili unavyohitaji, kitu ambacho hakitawezekana
ikiwa chakula tayari ni cha kumiminika.
Maziwa ya mama ni ya kumiminika ili yapite kwenye matiti
lakini yakifika tumboni mwa mtoto mara hugandishwa ili nayo yatulie na tumbo
lifanye kazi yake. Hatima ya vyakula vyote vyenye wanga tumboni na kwenye
utumbo ni sukari.
Vimeumbwa vile ili sukari ipatikane polepole kwa taratibu za mmengenyo
wa vyakula mwilini. Magamba yameingizwa kwenye nafaka na mboga mboga pia kwa
ajili hiyo.
Sukari ikiingia kwenye mwili kwa wingi huharibu sehemu nyingi
za mwili. Hivyo inashauriwa tusiongeze sukari kwenye vyakula. Matumizi ya
sukari yasizidi vijiko vya chai vitano kwa mtu kwa siku. Tusikoboe nafaka na
tule matunda yalivyo badala ya kutengeneza juisi.
Mlo wenye mboga mboga kwa wingi huongeza magamba kwenye
chakula na kupunguza kasi ya sukari kuingia mwilini.
Nani anaweza kuugua
kisukari
TDA inasema kwamba tafiti mbalimbali zilizofanywa hapa nchini
na duniani zimebaini kuwa mtu yeyote anaweza kupata ugonjwa wa kisukari.
TDA inaeleza kuwa tafiti zilizofanywa hapa nchini zimebaini
kwamba Watanzania tisa kwa kila 100 wenye umri wa miaka 25 na kuendelea
wanaugua ugonjwa wa kisukari.
Mbaya zaidi, TDA inaeleza kuwa kati ya hao tisa ni wawili tu
ambao wanajijua kuwa wanaugua kisukari. Wale wasiojijua huendelea kusishi na
kisukari kwa muda mrefu na hugunduliwa baada ya ugonjwa kusababisha madhara
makubwa mwilini yasiyofichika.
Hivyo watu wote wenye miaka 45 na kuendelea wanashauriwa
kupima afya angalau mara moja kila mwaka ili kugundua kama wana kisukari au
magonjwa mengine ambayo mwanzoni hayana dalili, kama vile msukomo wa juu wa
damu, magonjwa ya moyo, na hata saratani.
Hadi sasa, TDA inasema ugonjwa wa kisukari hauna dawa ila mtu
mwenye kisukari anaweza kuishi maisha marefu kama watu wengine ikiwa atafuata
ushauri wa wataalamu jinsi ya kuuthibiti ugonjwa.
Makala haya
yameandaliwa na:
Jukwaa la Waandishi wa Habari Wanaopambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TJNCDF), S L P 13695, Dar es Salaam. Baruapepe: tjncdf@gmail.com. Simu: +255 713 247889
SHARE
No comments:
Post a Comment