SERIKALI mkoani Mwanza imeitaka
jamii kote nchini kuwapeleka watoto wanaoishi na maambukizi ya virusi vya
ukimwi shule, badala ya kuwanyanyapaa na baadhi kuwaficha ndani na kisha
kufifisha ndoto zao za maisha.
Akizungumza katika kambi ya siku
tano mjini hapa, mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza Dk Leonard Subi kwenye ufunguzi
wa kambi hiyo iliyotayarishwa na taasisi
isokuwa ya serikali ya ‘Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative
(AGPAHI) na kuwakutanisha watoto wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi
kutoka mikoa ya Tanga, Simiyu na Mara, Subi amehimiza umuhimu wa malezi kwa
watoto
“Naamini kila mtoto ana ndoto zake
katika maisha lakini zaidi sana katika
kusoma na vipaji vingine endapo tu akisaidiwa kwa kujengewa mazingira rafiki
yakumwezesha kupata elimu bila bugudha, alisema Subi na kuongeza “Kila mtoto
ana haki ya kuishi, apate afya bora”.
Naye , mkurugenzi mtendaji wa
taasisi hiyo ya AGPAHI, Dr. Sekela Mwakyusa, alisema jukumu la taasisi hiyo
zaidi ni kutoa usaidizi kwa vituo vya afya vilivyopo katika serikali kuu pamoja
na serikali za mitaa kwenye huduma za afya hususan katika maswala ya HIV/UKIMWI,
sambamba na huduma za afya ya uzazi kwa mama na mtoto.
Mwakyusa alifafanua kuwa tangu
taasisi hiyo ilipoanzishwa mwaka 2011, imekuwa ikifanya kazi katika mikoa
miwili ya Shinyanga na Simiyu. Lakini toka mwezi Oktoba mwaka 2017 taasisi
imekuwa na kutoa huduma katika mikoa sita ikiwemo Mwanza, Mara, Geita na Tanga.
Amefafanua kwamba hadi kufikia
mwezi Machi 2017 walikuwa wamewafikia watu wenye maambukizi ya virusi vya
ukimwi wapatao 189,000 na kati ya hao 8,620 ni watoto wadogo ambao ndio
nguvu kazi ya taifa lijalo.
“Kwetu kama Taasisi ni kutoa
huduma shirikishi zaidi na kuhakikisha kwamba tunaondoa maambukizi ya virusi
vya Ukimwi kwa watoto na pia tunabaki na kizazi ambacho hakina UKIMWI.” Alisema
Ameongeza kwamba tayari wamefikia
asilimia tano ya watu wote ambao wanawahudumia wakiwa ni watoto ingawaje lengo
ni kufikia angalau asilimia kumi ya watoto na hivyo wanafanya jitihada zote
kuweza kuwapata wale watoto kwenye vituo vya afya na pia kwenye jamii.
Hata hivyo, AGPAHI inajukumu
la kuwafuatilia afya za akina mama wakiwa bado na uja uzito hadi wanapozaliwa
kuhakikisha kwamba wanapata huduma zote zinazostahili toka tu pale mama anapo
pata ujauzito.
“Wapo wale watoto ambao kwa bahati
mbaya mama hakuweza kutabulika kwamba ana matatizo na tunawakuta mara nyingi
tukiwa tumeenda kufanya kampeni za upimaji au kwenye vituo vya afya wanakuja na
tunawatambua.” alisema Mwakyusa.
Aidha alitoa wito kwa jamii kuwa
na ushirikiano kwani asilimia kubwa ya jamii
hasa akina mama hawana nafasi ya kufanya maamuzi kama vile kwenda kupata
huduma za afya kwa wakati, huku wakiahidi kuweka kambi ingine katika mkoa wa
Kagera itakayohusisha mikoa ya Mwanza, Geita na Shinyanga kwa lengo lakuzidisha
uelewa kwa jamii juu ya masuala ya afya katika miezi ijayo.
SHARE
No comments:
Post a Comment