Said Mwishehe
MGOGORO unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) unatokana na wao wenyewe.
Aidha kwa kujua au kutofahamu. Nimekuwa nikifuatilia kwa muda mrefu kauli ambazo zinatolewa na upande wa Katibu Mkuu wao, Maalim Seif Sharif Hamad na watu wake na zile zinazotolewa na Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba.
Kwa kifupi wanachekesha lakini baya zaidi wanakera na wanaudhi. Wanayoyafanya unajiuliza dhamira yao ni ipi. Ni kuijenga CUF au kuibomoa?
Profesa Ibrahim Lipumba
Majibu watakakuwa nayo wenyewe na hasa Profesa Lipumba na Maalim Seif. Sina shaka na uwezo wao katika siasa za Tanzania na dunia kwa ujumla.
Wamekuwepo kwa miaka mingi na kubwa zaidi wameshika nafasi walizonazo kwa muda mrefu. Wanachama wamejenga imani kubwa kwa viongozi hao.
Ikafika mahali wanachama wakaamini hakuna anayeweza kuwa Katibu Mkuu ndani ya CUF zaidi ya Maalim Seif.
Pia wakaamini hakuna mwenye uwezo wa kuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa zaidi ya Profesa Lipumba. Wakawa wanajenga chama na wakafanikiwa. Kwa sasa mambo ni tofauti kabisa, ndani ya CUF sasa ni vipande vipande.
Maalim Seif na watu wake na Profesa Lipumba naye na watu wake.Ni aibu lakini wameitaka wenyewe.Wameharibu umoja na mshikamano wao bila sababu ya maana.
Nafahamu msingi mkubwa wa CUF kuingia kwenye mgogoro ambao haijulikani mwisho wake ni lini ulianza wakati wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Sababu kubwa ni kwenye urais. Tunafahamu wakati tunaelekea kwenye uchaguzi huo vyama vinne vya siasa viliamua kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Umoja huo msingi wake ulianza wakati wa mchakato wa Katiba Mpya ambayo nayo haikupatikana. Hivyo wapinzani wakawa wanashirikiana katika kujenga hoja kwenye mchakato wa Katiba mpya.
Umoja ule ambao waliuonesha wakaamini utawavusha kwenye uchaguzi mkuu. Hivyo wakautangaza rasmi katika Viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.
Hivyo kuanzia hapo wafuasi wa vyama hivyo wakawa kitu kimoja. Wakawa na vikao vya mikakati. Upepo ndani ya Ukawa ukabadilika ghafla baada ya Chadema kumkaribisha Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa aliyekuwa CCM.
Baada ya kufika Chadema wakamtangaza kuwa ndiyo mgombea urais wao na ndiyo anawakilisha Ukawa. Hali ya hewa ikachafuka kwa wale waliokuwa nao wanautaka urais kupitia umoja huo.
Miongoni mwao ni Profesa Lipumba. Najua alikuwepo na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Willibrod Slaa. Ndoto zao za urais zikagonga mwamba baada ya ujio wa Lowassa.
Hapo ndipo CUF ilipoanza kuingia kwenye mgogoro hasa baada ya Prof.Lipumba kuamua kujiengua wakati tunaelekea uchaguzi mkuu. Mengi yakazungumzwa.
Kifupi Prof Lipumba hakufurahishwa na ujio wa Lowassa Ukawa. Hivyo akajiweka kando. Sote tukajua Prof. Lipumba amejiondoa rasmi kwenye nafasi yake maana aliandika barua ya kuomba kujiuzulu.
Kwa Ujinga Wangu sitaki kuelezea zaidi nini kiliendelea maana wote tunafahamu. Uchaguzi mkuu ukafanyika na mgombea urais wa CCM Dk.John Magufuli akawa Rais.
Kumbe Prof.Lipumba alikuwa na akili yake kichwani, hivyo alitangaza kurudi kwenye nafasi yake ya uenyekiti kwa madai Maalim Seif alikuwa hajaandika barua ya kuridhia kujiuzulu kwake. Hivyo bado ni mwenyekiti halali.
Kwa Ujinga Wangu kwenye mgogoro huo utachukua muda mrefu kufika mwisho. Ninachokiona Prof Lipumba anatumia akili zaidi katika kukabiliana na akina Maalim Seif. Lipumba anajitahidi kutumia sheria, kanuni na taratibu za Katiba yao kujilinda.
Ninachokiona Kwa Ujinga Wangu upande wa Maalim Seif unatumia siasa zaidi kukabiliana na Lipumba. Wapo wanaosema Lipumba anabebwa na Serikali ingawa sina hakika.
Kwa Ujinga Wangu namuona Lipumba kama mwanasiasa asiyeyumba na mwenye kutumia elimu yake zaidi kuulinda uenyekiti wake.
Kila hatua anafuata sheria za vyama vya siasa nchini, anafuata Katiba ya CUF na miongozo mingine ya Serikali. Kwa kifupi Lipumba atawasumbua akina Maalim Seif.
Kwa namna ambavyo Prof Lipumba anapambana kwenye mgogoro huo Maalim Seif anatakiwa kutuliza akili yake. Kinyume cha hapo atakuwa na wakati mgumu.
Nikiri Maalim Seif ni mwanasiasa ambaye naye huwa hakubali kushindwa. Hivyo wote wamekutana maana Lipumba naye huwa hakubali kirahisi.
Kwa Ujinga Wangu niseme tu mgogoro unaondelea CUF unakolezwa na wana CUF wenyewe. Dawa ya kumaliza mgogoro huo anayo Maalim Seif na Lipumba.
Wenyewe ndiyo wanaweza kuumaliza kwani ni sawa na msemo wa kikulacho kinguoni mwako.
SHARE
No comments:
Post a Comment