Julian Msacky
NCHI yetu imeongozwa
na marais watano hadi sasa. Rais wa Awamu hii ya tano ni John Magufuli.
Kaulimbiu yake ni HAPA KAZI TU.
Awamu ya kwanza ya
Mwalimu Julius Nyerere ilijikita kwenye mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea. Ndiko
anakopita Rais Magufuli.
Rais John Magufuli
Baada ya Nyerere
alikuja Ali Hassan Mwinyi. Yeye kila kitu kilikuwa RUKSA. Wenye meno walikula
kwa ukali wa meno yao.
Alipoingia Rais wa
Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa akaja na dhana ya Uwazi na Ukweli. Kilichotokea
kila mtu anajua.
Mkapa alipoondoka
aliingia Jakaya Kikwete na kaulimbinu ya Kasi Mpya, Nguvu Mpya na Ari Mpya na
baadaye Maisha Bora Kila Mtanzania.
Kaulimbiu hizi
nitazijadili katika makala zijazo na namna gani zilifanikiwa au ziliacha watu porini
na kujikuta wakibembea angani.
Katika mada ya leo
itoshe kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefumbua Watanzania macho.
Serikali hii chini ya
Rais Magufuli umeonesha namna tunavyoibiwa rasilimali zao kila kukicha na
kimsingi hataki kuona tena hali hiyo.
Mfano nzuri tumeuona
kwenye sekta yetu ya madini ambako ufujaji mkubwa wa mapato unafanyika kwa
kiwango kikubwa.
Kama tulivyosikia ama
kuambiwa na Rais Magufuli ni kwamba kiwango tunachopata ni kidogo ukilinganisha
na kinachopotea.
Hii ina maana kuwa
Tanzania si maskini, lakini ni wa kujitakia ndiyo maana Rais anasema
“Watanzania tumelogwa na nani?
”
Katika safu hii ya leo
ninapenda kuzungumzia matumizi sahihi ya rasilimali za nchi katika kuharakisha
maendeleo yetu.
Ninazungumzia hili
baada ya kubaini kuwa rasilimali zetu nyingi hazitumiki ipasavyo ndiyo maana
tunashindwa kupiga hatua inavyotakiwa.
Kwa msingi huo
ninashauri ama kupendekeza mfumo unaofaa wa kutumia rasilimali zilizopo kukuza
sekta mbalimbali nchini.
Ninadhani umefika
wakati sasa tuweke utaratibu wa kutumia rasilimali mathani madini ya dhahabu
pekee kuhudumia sekta ya elimu.
Hii ikiwa na maana
kuwa mapato yanayotokana na madini kama nchi tunaweza kuamua ni kwa ajili ya
kuhudumia shule za msingi tu.
Kwa maana kuwa watoto
wasome bure, wapatiwe vitabu muhimu na vitendea kazi bora kwa walimu na
mazingira bora ya kufundishia.
Hatuna sababu ya
kuumiza vichwa namna gani watoto wetu wasome wakati tunao utajiri wa kutosha
kufanya mambo hayo vizuri.
Hatuna sababu ya
walimu kutolipwa vizuri au kukosa nyumba bora za kuishi wakati mali zetu zinasombwa
kama hazina wenyewe.
Tangu tumeanza
kuchimba madini hadi sasa ninaamini hatuna mfuko maalumu wa mapato hayo na
badala yake tunazitumia tunavyojua.
Mimi naamini tukiweka
mfumo wa kila rasilimali kuhudumia eneo fulani itasaidia kuliko ilivyo sasa
kwani tunapoteza vingi.
Hebu tujiulize kama
Libya chini ya Muammar Gaddafi alitumia mafuta kuifanya nchi hiyo na watu wake
kuishi vizuri, sisi tunashindwa nini.
Gaddafi alisomesha
wanafunzi hadi vyuo vikuu kwa mapato ya mafuta, akawajengea nyumba, akawapatia
umeme, maji na vingine vingi.
Alifanya hivyo kwa
kutumia rasilimali ya mafuta. Alitumia pia rasilimali hiyo kwa usahihi kusaidia
mataifa mengi tu ya Afrika.
Hicho ndicho
kilichowaudhi mabepari na kumuua. Hicho ndicho pia kilichosababisha Saddam
Hussein wa Iraq auawe.
Kwa hiyo utamaduni wa
kutumia mapato yatokanayo na rasilimali zetu kiholela utakoma endapo kila
rasilimali itahudumia upande wake.
Tunaweza kufanya hivyo
kwa majaribio chini ya usimamizi imara na kuangalia je, dhahabu inamudu
kuendesha sekta ya elimu?
Hili linawezekana kwa
sababu Rais Magufuli alipoingia madarakani amefanya mabadiliko makubwa na
mafanikio yanaonekana.
Kwa mfano, alisimamia
suala la upungufu wa madawati shuleni na leo hii nadhani hakuna shule yenye
tatizo hilo kwa kiwango kikubwa.
Alianzisha kampeni ya
usafi na hadi sasa inaendelea ingawa baadhi ya mikoa, ikiwemo Dar es Salaam
hali bado si nzuri.
Hii maana yake ni
nini. Maana ni kuwa tuna tatizo la uongozi kuanzia idara moja hadi nyingine
ndiyo maana tunakwama.
Kwa hiyo Rais amezibua
mirija ambayo iliziba ndiyo maana tunaona mambo yanakwenda. Hii ni changamoto
nyingine.
Ni kwa hiyo njia
tunatakiwa tuanze kuweka mifumo ambayo itasaidia kuboresha huduma zetu za
kijamii kwa kutumia rasilimali asilia.
Kama utajiri wa
kutosha tunao ni kwani tusijiwekee utaratibu wa kila rasilimali iliyopo nchini
ishughulike kutatua jambo fulani.
Utajiri uliopo hatuna
sababu ya wananchi kukosa huduma bora za afya. Uwezo wa serikali kuwapitia huduma
nzuri upo.
Kwa utajiri tuliona
nao tuna uwezo wa kutoa tiba bure kwa Watanzania. Mathalan tukitenga mapato
yatokana na misitu tutashindwa nini.
Mlima Kilimanjaro
umetuingizia mapato mangapi tangu tupewe bure na Mwenyezi Mungu? Hayatoshi
kuhudumia sekta ya afya?.
Wakati tuna chanzo
hiki, hebu tujiuze ni kwa nini tuangalia wananchi wakifa, wakiwemo wajawazito
kwa kukosa huduma bora.
Hivi kweli tulistahili
kukosa zahanati, vituo na hospitali za kutosha nchini kwetu au ni kwa sababu tu
ya kusimamia rasilimali zetu vibaya.
Tulistahili kweli kuwa
na shule zisizo na vyoo katikati ya utajiri uliopo nchini au ni matumizi holela
ya utajiri tuliopewa na Mungu?
Inabidi tuseme
imetosha. Kama wazungu wanatumia mali hizi hizi kufanya mataifa yao yaonekane
kama peponi, tunashindwa nini.
Leo hii ukienda
Marekani inang’aa. Ukienda Uingereza inang’aa. Ukienda Canada vivyo hivyo. Hivi
tatizo letu ni nini?
Ni lazima tubadilike.
Ni lazima viongozi nao wabadilike na kutuonesha kuwa Tanzania inaweza kuwa kama
Marekani. Naam.
Haiwezekani mali zetu
zineemeshe mataifa mengine halafu tukimbilie kwao kwenda kutibiwa kwa sababu
eti wana hospitali nzuri.
Tuna mali za kuweka
hospitali hizo. Ni wapi tuanzie ndiyo mjadala tunaofungua hapa. Ninaamini
tukiamua inawezekana.
SHARE
No comments:
Post a Comment