Na Joachim Mushi, Babati
MKUU wa Wilaya ya Babati, Raimond
Mushi amewataka wakulima kufuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo
wakiwemo watafiti wa mbegu bora chotara za mahindi zinazostahimili
ukame, magonjwa (WEMA) ili waweze kuendesha kilimo chenye tija na
kuachana na kilimo cha kujikimu ambacho hakiwezi kuwapa maendeleo.
Alisema kilimo cha sasa kinapaswa
kuendeshwa kisayansi na kufuata ushauri wa kitaalamu, ambapo ni pamoja
na kutumia mbegu bora zilizofanyiwa utafiti kulingana na mahitaji ya
maeneo ya wakulima. Mh. Mushi ametoa ushauri huo mjini Babati alipokuwa
mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Wakulima wilayani Babati
ambapo pia alitembelea shamba la utafiti shirikishi wa mbegu za mahindi
unaotekelezwa na watafiti kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa
ushirikiano na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia
mradi wa utafiti wa mbegu bora chotara za mahindi zinazostahimili ukame
na magonjwa (WEMA).
Alisema wakulima wakitaka kufanya
kilimo cha manufaa hawana budi kutumia mbegu zilizofanyiwa utafiti na
kupendekezwa na wataalamu wa kilimo kutumika katika maeneo yao. “…Tuwe
macho na mbegu tunazonunua ili tuweze kuvuna mazao ya kutosha, wakulima
sasa lazima tubadilike tusiendeshe kilimo cha kujikimu tu…mkulima huwezi
kuendelea kwa kufanya kilimo cha kujikimu, tunataka ulime upate chakula
na ziada kisha uuze mazao kukuza uchumi wako na ubaki na akiba,”
alisema Raimond Mushi.
Alisema serikali ya awamu ya nne
imedhamiria kufanya uchumi wa viwanda hivyo wakulima wanakila sababu ya
kufanyia kazi ushauri wa wataalamu wa kilimo ili waweze kuzalisha mazao
ya kutosha yatakayotumika kama mazao ghafi kwenye viwanda na kunufaika
zaidi.
“Tunapolima sasa tulime kisayansi
na kwa malengo, tutumie maeneo yetu vizuri ili tuweze kuzalisha mazao
ya kutosha,” alisisitiza Mkuu wa Wilaya, Raimond Mushi na kuongeza eneo
la kilimo kwa sasa linapungua kutokana na ongezeko la idadi ya watu
nchini hivyo kuna kila sababu ya kutumia eneo dogo linaloleta matokeo
makubwa na manufaa kwa mkulima.
Alisema serikali imedhamiria
kuleta mabadiliko kwa wakulima ndio maana inawawezesha wataalamu kama
WEMA na kuwaunga mkono shughuli za utafiti kwa maendeleo ya wananchi
hawa wakulima. “Sisi hapa Babati tunangoja kwa hamu matokeo ya utafiti
ili tuweze kuyafanyia kazi…tuleteeni mapema tutasimamia na kuhamasisha
wakulima wetu kutumia mbegu za WEMA,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Msaidizi wa Kitengo cha Maendeleo ya Utafiti kutoka Wizara ya Kilimo
Mifugo na Uvuvi, Jackson Nkuba alisema Serikali ipo tayari kushirikiana
na makampuni yatakayojitokeza kuzalisha mbegu za WEMA na zingine bora
zinazofanyiwa utafiti ili wakulima wazipate kirahisi, hivyo kutoa rai
kujitokeza kwa wingi.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Babati,
Bw. Mushi, viongozi mbalimbali katika tukio hilo wakiwemo wakulima kwa
pamoja walitembelea shamba la utafiti shirikishi wa mbegu bora chotara
za mahindi zinazostahimili ukame na magonjwa (WEMA) lililopo Mtaa wa
Maisala Kata ya Babati Mjini na kujionea mbegu zilizofanyiwa utafiti wa
WEMA na kujionea matokeo ya utafiti.
SHARE
No comments:
Post a Comment