Mh. Zelote Stephen (mwenye
miwani) akioneshwa kitanda cha kujifungulia na RMO Dk. Boniface Kasululu
muda mfupi kabla ya kuvikabidhi kwa Wakuu wa Wilaya. kutoka kushoto ni
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura akifuatiwa na Katibu
tawala wa Mkoa Bernard Makali.
……………………………………………………………………..
Katika kuendeleza dhana ya
maendeleo hayana chama Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote
Stephen amewashirikisha madiwani wa chama cha CHADEMA katika harambee ya
ghafla iliyolenga kumalizia ujenzi wa jengo la huduma za afya ya uzazi
na mtoto katika kituo cha afya Mazwi, Manispaa ya Sumbawanga.
Harambee hiyo ilifanyika muda
mfupi kabla ya Mh. Zelote Kukabidhi jumla ya vitanda vya kujifungulia
16, vitanda vya wagonjwa 80, magodoro 80 pamoja na mashuka 200 kwa wakuu
wa wilaya ikiwa ni sehemu ya mgawo wa vifaa hivyo uliofanyika nchi
nzima kupitia juhudi za Rais Dk. John Pombe Magufuli katika kuimarisha
huduma za uzazi nchini.
Akiongea mbele ya wananchi
waliohudhuria katika tukio hilo Mh. Zelote alisema kuwa serikali ya
awamu ya tano sio ya maongezi bali vitendo hivyo kuwataka waheshimiwa
madiwani sita wakiwemo watatu wa CHADEMA wakiongozwa na Meya wa Manispaa
ya Sumbawanga kuchangia ujenzi wa jengo hilo jipya ili kuboresha huduma
kwa wananchi waliowachagua.
“Ili Manispaa iwe jiji tunahitaji
huduma bora katika kituo hiki hivyo basi, Mimi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,
Zelote Stephen nachangia tani tano za “cement” ambayo ni mifuko 100,”
alitangulia kusema.
Harambee hiyo ilikusanya ahadi ya
vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 5.5 huku jengo hilo likiwa
limegharimu Shilingi Milioni 16 hadi kusimama.
Awali akisomewa taarifa kabla ya
kuzindua huduma ya kujifungua iliyoanza tarehe 1/7/2017 katika kituo
hicho afisa muuguzi Mariam Kidya alieleza kuwa jengo lililopo la huduma
ya afya ya uzazi na mtoto lina uwezo wa kuhudumia kina mama 2,327 lakini
kwa mwaka 2016/2017 limeweza kuhudumia kina mama 31,257 jambo
lililopelekea kuanzisha ujenzi wa jengo jipya ili kuimarisha utoaji wa
huduma kwa akina mama.
Aidha Mh. Zelote aliwasisitiza
wananchi kuendelea kulipa kodi ili kuendelea kuboresha huduma na kuleta
maendeleo katika sekta mbalimbali nchini na kuonya kuwa wale
watakaolipishwa ili kupata huduma ya afya ya uzazi na mtoto basi wafike
ofisini kwake ili achukue hatua.
“Ndio maana Mheshimiwa Rais
amesisitiza sana watu tulipe kodi wote ili kutatua kero mbalimbali za
wananchi hususan watu wa hali ya chini. Nataka nisisitize ulipaji wa
kodi ili kazi kama hii na zingine zifanyike.
Kwa upande wake mganga mkuu wa
mkoa Dk. Boniface kasululu alipokuwa akisoma taarifa ya huduma ya afya
na uzazi ya mkoa, alisifu uamuzi wa Rais Dk. John Pombe Magufuli wa
kununua vifaa hivyo kupitia bohari kuu ya dawa (MSD) kwani changamoto
hizo zimekuwa zikiwasumbua kwa muda mrefu kuanzia ngazi ya mkoa hadi
katika halmashauri.
“Sekta ya afya kukabiliwa na
changamoto kadhaa kubwa ikiwa ni upungufu wa vifaa na vifaa tiba muhimu
na ufinyu wa miundombinu ya kutolea huduma kwa maana ya majengo, hivyo
tunapongeza juhudi za rais wetu mpendwa kutupatia vifaa hivi na
tunaahidi kuvitunza ili viweze kuwasaidia kina mama wa mkoa wetu,”
Alisema.
SHARE
No comments:
Post a Comment