I
Jeshi
la Magereza nchini limeanza kutekeleza mpango wake wa kupanua shughuli
za uzalishaji wa kiwanda cha Viatu cha Karanga kilichopo mjini Moshi
mkoani Kilimanjaro sambamba na kujenga kiwanda kipya cha viatu katika
eneo hilo hilo ili kupanua huduma zake kwa wananchi na hivyo kukidhi
mahitaji ya soko la sasa.
Hatua
hii ni moja ya kati ya Mikakati ya Jeshi la Magereza nchini Tanzania
linaloongozwa na Kamishna Jenerali Dk. Juma Malewa kuhakikisha fursa
zilizopo na wataalamu waliopo ndani ya Jeshi la Magereza nchini
zinatumika na wanatumika vizuri kwa manufaa ya watanzania wote sambamba
na Jeshi hilo kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha Tanzania inafikia
uchumi wa viwanda.
Kamishna
Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dr. Juma Malewa anasema baada ya
upanuzi huo ambao umeanza kufanyika mapema mwezi Juni mwaka huu kiwanda
hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha jozi 400 kwa siku na hivyo
kuongeza kasi ya upatikanaji wa viatu vinavyotengenezwa na Jeshi la
Magereza kwa ubora kwa hali ya juu na kwa kutumia mitambo ama mashine
za kisasa.
Dk.
Malewa anasema awali kiwanda hicho kilichopo Gereza la Karanga mjini
Moshi Mkoani Kilimanjaro kutokana na kutumia teknolojia ya zamani
kilikuwa na uwezo wa kuzalisha jozi 150 kwa siku kiwango ambacho ni
kidogo ukilinganisha na soko la sasa.
Anasema
tayari Jeshi la Magereza limeingia Ubia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa
PPF kwa lengo la kupanua shughuli za uzalishaji wa Kiwanda cha
Viatu cha Karanga kilichopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro sambamba na
kujenga kiwanda kipya cha viatu katika eneo hilo hilo.
Dk.
Malewa anasema katika kutekeleza azma yake ya ujenzi wa Kiwanda kipya
cha Viatu tayari zimetengwa ekari 20 kwa ajili ya kiwanda hicho katika
eneo hilo la Karanga mjini Moshi na kwamba eneo hilo hilo litakalotumika
kujenga Kiwanda cha Viatu pia litatumika kujenga Kiwanda cha Soli na
Kiwanda cha kuchakata Ngozi na kwamba Kiwanda hicho kinategemewa
kukamilika mapema Julai mwaka 2018.
Katika
kuinua hali ya uchumi kwa watanzania “Uzalishaji huu utaongeza ajira
kwa watanzania, lakini pia utaongeza soko la uuzaji wa viatu hivi kwa
kuwa tunategemea kutengeneza viatu kwa wingi kwa ajili ya Majeshi yetu
yote ya Tanzania pamoja na viatu kwa ajili ya shule za Sekondari za
Serikali kwa hiyo hii ni fursa nzuri na kubwa katika Jeshi letu la
Magereza”. anasema Dk. Malewa.
Dk.
Malewa anasisitiza kuwa sambamba na upanuzi wa Kiwanda kilichopo
Gereza la Karanga mjini Moshi pia Jeshi la Magereza limeanza upanuzi
wa Viwanda vya Samani vilivyopo Ukonga, Arusha na Tabora ili viweze
kuongeza uzalishaji wa samani kwa ajili ya matumizi ya ofisi mbalimbali
na majumbani.
Katika
mwendelezo wa kupanua viwanda vyake ili viweze kuwa na tija kwa taifa
na watanzania kwa ujumla kwa sasa Jeshi la Magereza nchini kwa kutumia
rasilimali zake lina mpango wa kujenga Kiwanda Kikubwa cha Uzalishaji wa
Samani ambacho kitaweza kuhudumia watanzania kwa kiwango kikubwa na
tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda hicho
ambacho kitajengwa mkoani Dodoma.
“Kutokana
na Serikali kuhamishia Makao Makuu ya Nchi yetu Mkoani Dodoma ni wazi
kutakuwa na uhitaji mkubwa wa samani kwa ajili ya matumizi ya ofisi na
hata majumbani pia… hivyo tunategemea Jeshi la Magereza litajenga
Kiwanda hiki kikubwa cha samani ili kukidhi mahitaji halisi ya samani
hizo kwa watanzania wote na taasisi mbalimbali zilizopo mkoani Dodoma
,’’ anasema Dk. Malewa.
Dk.
Malewa anasema ili kukidhi mahitaji halisi samani kwa ajili ya Makao
Makuu ya Nchi yetu Jeshi la Magereza lina mpango wa kununua vifaa
hususani mashine za kisasa zitakazoweza kuzalisha samani kwa wingi
zaidi na hivyo kutosheleza mahitaji ya samani mjini Dodoma.
Kwa
mujibu wa Dk. Malewa nguvu kazi itakayotumika katika uzalishaji kwenye
kiwanda hicho itakuwa ya aina mbili ikiwemo wataalamu waliopo ndani ya
Jeshi la Magereza na wananchi ambao wataajiriwa kutokana na utaalamu
walio nao, hivyo Jeshi la Magereza linatarajia kuongeza fursa za ajira
kwa wastani wa ajira 200 hadi 500.
Katika
kuhakikisha Jeshi la Magereza nchini linapanua wigo wa utoaji wa huduma
zake kwa taifa Jeshi la Magereza linategemea kuingia ubia na GEPF
ili kutekeleza mradi wa upasuaji kokoto utakaofanyika mkoani Dodoma.
Kwa
mujibu wa Dk. Malewa Jeshi la Magereza linategemea kufunga mashine
kubwa ya upasuaji wa kokoto ambapo kwa kiasi kikubwa inategemewa kukidhi
mahitaji ya kokoto katika shughuli za ujenzi wa nyumba za wananchi hata
Mashirika mbalimbali yanayohamia mkoani Dodoma.
Dk.
Malewa anasema, kwa kuwa tayari ujenzi wa nyumba za Taasisi na watu
mbalimbali unaendelea kutekelezwa mkoani Dodoma, kupitia Mradi wa
upasuaji wa Kokoto unaofanyika katika eneo la Msalato mkoani humo,
kokoto hizo zitauzwa kwa watu binafsi yaani wananchi na Serikali pia.
Dk.
Malewa anasema Jeshi la Magereza ni Taasisi kubwa ambayo ina fursa
nyingi za kiuchumi na endapo zitatumiwa vizuri zinaweza kuwa na mchango
mkubwa kwa Taifa hili ambalo linaelekea kwenye uchumi wa viwanda.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja
Jenerali Projest Rwegasira anasema kuwa pamoja na Jeshi la Magereza
nchini kutumia wataalamu wake pamoja na wafungwa ambao hufundishwa stadi
mbalimbali na kutumika kama nguvu kazi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania imeendelea kuthamini na kuunga mkono juhudi mbalimbali
zinazoonyeshwa na Jeshi la Magereza ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa
na Jeshi hilo hapa nchini yanatekelezwa kama yalivyokusudiwa.
Kwa
upande wake mwananchi mmoja Crispin Aloyce Mkazi wa Ubungo jijini Dar
es Salaam anasema yeye ni mtumiaji na mteja mzuri wa viatu vya ngozi
vinavyozalishwa na Jeshi la Magereza nchini na amekuwa akinunua viatu
hivyo kwenye Duka la Magereza lililopo Mtaa wa Uhindini jijini Dar es
salaam, ‘‘Ni kweli viatu vyao ni vizuri na vina ubora wa hali ya juu,
ila Magereza wanapaswa kuzalisha kwa wingi viatu vya rangi ya ‘‘brown’’
ambayo watu wengi pia tunaipenda imekuwa ni kawaida mteja unapotaka
viatu vya rangi ya ‘brown’ unaambiwa rangi hiyo imeisha… haiwezekani
kila siku unakosa rangi hii’’ anasema Bw. Aloyce.
SHARE
No comments:
Post a Comment