FRANK
MVUNGI –MAELEZO
WAZIRI
wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba (Mb)
ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Usimamizi
wa Mazingira (NEMC) na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ili kuongeza tija na
kutekeleza kwa vitendo dhana ya Ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Kwa
kuzingatia mamlaka aliyonayo Waziri
chini ya Sheria ya Mazingira kifungu cha 19 (2) anaweza kutengua uteuzi wa
Mkurugenzi wa Baraza hilo na wajumbe wake.
Akizungumza
na vyombo vya Habari jana jijini Dar es Salaam Waziri Makamba amesema kuwa lengo
la mabadiliko hayo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na usimamizi na uzingatiaji wa
Sheria ya Mazingira na uharakishaji wa
miradi ya maendeleo na uwekezaji hasa ujenzi wa viwanda kama azma ya Mheshimiwa
Rais John Magufuli inavyoelekeza.
Kufuatia
mabadiliko hayo Waziri Makamba amemteua Dkt. Elikana Kalumanga ambaye ni
Mhadhiri katika Taasisi ya Usimamizi na Tathmini ya Rasilimali Asili,Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC hadi Rais atakapoteua Mkurugenzi
Mkuu.
“Utendaji
wa NEMC umekuwa ukilegalega sana na umekuwa hauridhishi na kumekuwepo na
malalamiko mengi kutoka kwa wawekezaji
wa ndani na nje ya nchi kuhusu ucheleweshaji na urasimu usiokuwa wa
lazima katika mchakato wa tathmini ya athari kwa mazingira (EIA)” Alisisitiza
Mhe. Makamba
Aliongeza
kuwa ametengua uteuzi wa wajumbe wote saba wa Bodi ya NEMC ili baadaye ateue
wajumbe wapya ambao wataendana na kasi na ari ya Serikali ya Awamu ya Tano
katika kuelekea uchumi wa Viwanda, ambapo Mwenyekiti wa Bodi ambaye mamlaka
yake ya uteuzi ni Mheshimiwa Rais,ataendelea kuwepo hadi Mheshimiwa Rais
atakapoteua mwingine.
Akifafanua
Makamba amesema kuwa changamoto nyingine zilizobainika ni kuwaelekeza
wawekezaji kwa makampuni ya kufanya Tathmini ya athari za mazingira ambayo
yanamilikiwa au yenye ubia na watumishi wa NEMC, bila kujali mgongano wa
kimaslahi jambo ambalo haliruhusiwi katika utumishi wa umma.
Jambo
jingine ni kuwarundikia maandiko ya miradi ya tathmini ya athari kwa mazingira
(EIA) watumishi wachache wakati wengine hawana kazi ili waelekeze miradi hiyo
katika makampuni ambayo baadaye huwapatia malipo yasiyo halali.
Hatua
nyingine zilizochukuliwa na Waziri Makamba ni pamoja na kuiagiza NEMC kufuta
watu binfsi na Makampuni yote ya ushauri wa EIA (Consultants) ambayo hayana
sifa au yameshindwa kutekeleza kazi zao vizuri na watangaze kwenye magazeti orodha ya watu na makampuni yanayoruhusiwa
kufanya kazi kama washauri elekezi.
Baraza
la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC ni muhimu katika kuhakikisha
ustawi wa mazingira na mustakabili wa maendeleo endelevu ya nchi tunapoelekea
kuwa Taifa la uchumi wa viwanda lazima usimamizi wa mazingira uwe thabiti.
SHARE









No comments:
Post a Comment