Aliyekuwa waziri
mwenye uwezo mkubwa katika utawala wa aliyekuwa rais wa pili nchini
Kenya, Daniel Toroitich Arap Moi , Nicholas Biwott amefariki dunia.
Nicholas Biwott
Alipelekwa katika hospitali ya Nairobi Hospital lakini mwendo wa saa tatu asubuhi akaaga dunia.
Biwott hatahivyo alikuwa akiugua kwa muda mrefu huku ripoti za uongo kwamba amefariki zikitolewa awali kabla ya kifo chake.
Bowott ambaye aliwahi kuhudumu kama mbunge wa Keiyo na kiongozi wa chama cha National Vision Party hivi majuzi alitangaza kwamba chama chake kitaunga mkono kuchaguliwa tena kwa rais Uhuru Kenyatta.
Biwott alizaliwa katika kijiji cha Chebior, wilaya ya Keiyo katika mkoa wa Rift valley 1940.
Aliwahi kuhudumu kama mwanachama wa bunge la Kenya kwa miaka 28, baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza 1974 kama mbunge wa Keiyo Kusini hadi mnamo mwezi Disemba 2007, wakati alipopoteza kiti chake kwa Jackson Kiptanui wa chama cha ODM.
Kufuatia kuchaguliwa kwake mwaka 1979, Biwott alihudumu kama waziri wa maswala ya taifa akisimamia idara za Sayansi na Teknolojia vile vile waziri wa maswala ya ardhi na kilimo cha unyunyizaji.
Mara ya mwisho kuhudumu waziri ilikuwa 2001-2001 ambapo alihudumu kama waziri wa maswala ya biashara, viwanda na utalii wa Afrika mashariki wakati wa utawala wa aliyekuwa rais Daniel Moi.
Waziri huyo wa zamani na mfanyibiashara alikumbwa na utata wakati wake.
Biwott alitajwa na jasusi wa Scotland yard John Troon kama mtu muhimu katika kifo cha aliyekuwa waziri wa maswala ya kigeni nchini Kenya Robert Ouko 1990.
Maofisa 10 wa serikali akiwemo Biwott walikamatwa na polisi na kuhojiwa kwa wiki mbili mnamo mwezi Novemba 1991, lakini uchunguzi wa maafisa wa polisi ulikamilika ukikosa ushahidi kwamba Biwott alihusika kwa kutoweka na hatimaye kifo cha Ouko.
CHANZO: BBC
SHARE
No comments:
Post a Comment