Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
imetangaza kutoa vibali vya ajira 10,184 ili kuziba nafasi zilizoachwa
wazi na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu,
imefahamika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais, Utumishi, Florence Temba, ilieleza
kuwa agizo hilo linazihusu Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekretarieti
za Mikoa, Wakala wa Serikali, pamoja na Taasisi na Mashirika ya Umma.
Ilimnukuu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki akitoa agizo hilo wakati
akizungumza katika kikao kazi na watumishi wa Umma wa Wilaya ya
Kigamboni mkoani Dar es Salaam jana.
“Mgawanyo wa vibali vya ajira umezingatia upungufu uliojitokeza
baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki, vipaumbele vya Taifa kwa sasa
na upatikanaji wa watumishi kutoka katika soko la ajira,” alisema Kairuki.
Kairuki aliongeza kuwa taratibu za kukamilisha mgawo wa nafasi za
ajira 4,816 zilizosalia unaendelea ili kuwezesha wizara na taasisi
nyingine zilizokamilisha uhakiki wa watumishi wa umma hivi karibuni
kuajiri watumishi wapya kuziba nafasi wazi zilizojitokeza.
Alieleza kuwa serikali imetoa kibali kuajiri watumishi wapya 15,000
ili kuziba pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye orodha ya malipo
ya mishahara kwa watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti baada ya
zoezi la uhakiki.
“Watumishi wa umma watakaoajiriwa kuziba nafasi hizo wanatarajiwa kuripoti kazini kuanzia mwezi Agosti, 2017,”
alieleza Waziri Kairuki, na kuongeza kuwa utaratibu wa ajira mpya za
serikali upo palepale na amewataka wananchi kutokuwa na wasiwasi wowote
wa ajira hizo.
“Napenda kusisitiza kuwa vibali tulivyovitoa leo ni vile
vilivyoziba pengo la walioghushi vyeti, naomba wananchi watambue kuwa
suala la ajira mpya bado liko pale pale kama serikali ilivyojipanga,” alisema Kairuki.
Aprili mwaka huu, Rais John Magufuli alipokea ripoti yenye orodha
ya watumishi wa umma ambao kati yao wanadaiwa kuwa na vyeti pungufu,
vyenye utata na vya kughushi kutokea kwa Waziri Kairuki.
Waliokuwa na vyeti vya kughushi walikuwa 9,932, na Rais aliapa
kwamba hawatarudi kazini. Rais Magufuli aliagiza kufutwa kazi kwa wote
waliotajwa kwenye ripoti hiyo na kuzuia mishahara yao ya mwezi huo,
lakini hata hivyo bado mlango uliwekwa wazi kwa wenye pingamizi na wapo
waliokataa rufaa huku wengine wakienda kwenye mamlaka husika kutafuta
ufumbuzi wa suala hilo.
Wiki iliyopita akiwa Dodoma, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro
alitangaza kuwa wiki hii serikali itatoa vibali 3,000 vya ajira katika
sekta ya afya vikiwemo vya madaktari na wauguzi pamoja na maofisa hesabu
535 kwa ajili ya vituo vya afya vya kata ili washughulike na ukusanyaji
wa mapato kwenye vituo vya afya na zahanati.
SHARE
No comments:
Post a Comment