Taharuki imewakumba wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Songwe (SIA) mkoani Mbeya na wananchi wanaofanya shughuli kando mwa
barabara kuu ya Tanzania -Zambia baada ya moto kuwaka ndani ya eneo la
uwanja huo.
Moto ambao chanzo chake bado hakijafahamika ulitokea jana mchana na
kaimu meneja wa uwanja huo, Jordan Mchami alisema iliwachukua takriban
nusu saa kuuzima.
Alisema moto huo ulianzia katika eneo la barabara kuu ya Tanzania -
Zambia umbali wa mita 600 kutoka maeneo yalipo majengo na eneo la
kurukia ndege.
“Tumefanikiwa kuuzima, hakuna madhara yoyote katika eneo letu na si
sahihi kusema uwanja umeungua. Ifahamike kwamba uwanja huu una eneo
kubwa ambalo ni kama vile pori tu. Moto umetokea barabara kuu ya
Tanzania -Zambia umbali wa mita 600 hivi hadi tulipo sisi,” alisema
baada ya kuenea taarifa katika mitandao ya kijamii na maeneo ya jirani
kwamba uwanja huo umewaka moto.
Alipoulizwa kuhusu cha moto huo Mchami alisema ulionekana kuanzia
barabarani na walipofuatilia kwa kuwauliza kina mama wanaofanya biashara
ndogondogo kando mwa barabara hiyo waliambiwa kuwa waliona lori
lililokuwa limeegeshwa eneo ulikoanzia hivyo wanahisi huenda mtu au watu
waliokuwa katika gari hilo walirusha kipande cha sigara na kusababisha
nyasi kuwaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga alipotafutwa kuzungumzia
suala hilo, simu yake ilipokewa na msaidizi wake aliyesema kamanda yupo
kwenye msafara wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Hata hivyo, taarifa za ofisa mmoja wa polisi aliyekuwapo eneo la tukio
ambaye aliomba jina lake lisiandikwe kwa kuwa si msemaji
alisema,“Tumefanikiwa kuuzima moto ambao ulienea eneo kubwa. Tunashukuru
haukuweza kufika maeneo ya kurukia ndege au kuharibu mali za uwanja
huu.”
Uwanja huo umeongeza wigo wa fursa za kibiashara na kurahisisha huduma
za usafiri wa anga kwa wakazi wa Mbeya, huku ukianza kuunganisha Kanda
ya Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine duniani.
Kadri siku zinavyokwenda, watu kutoka nchi jirani za Zambia, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Malawi wamekuwa wakiutumia uwanja huo.
Wageni hao ambao huingia nchini kwa ajili ya shughuli za biashara na
utalii, wamezidi kuifungua kibiashara mikoa ya Songwe na Mbeya na
kuonyesha ishara chanya kuwa uwanja huo unaelekea kuwa kitovu cha
biashara kati ya Tanzania na nchi za kusini mwa Afrika.
SHARE
No comments:
Post a Comment